
LEO mbivu na mbichi ya timu ya taifa, Taifa Stars itajulikana baada ya kumalizika mchezo wake wa marudiano dhidi ya Uganda ‘The Cranes’ utakaopigwa Uwanja wa St. Mary’s jijini Kampala.
Stars itakuwa ugenini ikihitaji ushindi ili ifuzu kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) baada ya kufungwa bao 1-0 kwenye mechi ya awali iliyopigwa wikiendi iliyopita Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Timu hiyo itaingia kwenye mtanange huo ikiwa na benchi jipya la ufundi baada ya Kim Poulsen raia wa Denmark kufungashiwa virago baada ya kufungwa na Uganda. Na sasa mikoba hiyo ipo chini ya Mzambia, Honour Janza akisaidiana na Mecky Maxime na kocha wa makipa, Juma Kaseja.
Benchi hilo limeingia wakati ambao Tanzania ipo kwenye mtihani wa kutaka kufuzu michuano hiyo inayotarajia kufanyika Algeria mwakani, lakini pia wakihitaji kurejesha imani ya timu hiyo hasa baada ya kuonesha kiwango kibovu wikiendi iliyopita.
Hata hivyo, mashabiki wengi wameonesha kuvutiwa na uteuzi huo kulingana na wasifu wa makocha hao huko walikotoka na hata wakati wakisakata kabumbu la ushindani.
Janza amechukuliwa kutoka Namungo, timu yenye ushindani kwa vigogo na imekuwa ikisumbua Ligi Kuu Bara tangu imepanda daraja na hata msimu huu haijaanza vibaya kwa maana ya sare ya mabao 2-2 na Mtibwa Sugar kabla ya kuifumua Ihefu bao 1-0.
Uwepo wa wachezaji wengi wazawa kwenye kikosi cha Namungo, inatoa mwanga kwa Janza kufahamu sifa za wachezaji wa Tanzania na namna ya kufanya nao kazi hasa kwenye mazingira yanayohitaji ushindi kwa nguvu zote kama ilivyo sasa.
Inaelezwa Janza alikuwa miongoni mwa makocha wasaidizi wa timu ya taifa ya Zambia chini ya kocha Herve Renard wakati ikitwaa ubingwa Afcon 2012, hivyo kuna hazina ya ushindani na ushindi kwenye benchi la Stars.
Kuhusu Maxime, kila mmoja anafahamu weledi wake na jitihada zake katika ukocha na uzalendo wake kwa wachezaji wazawa hivyo uwepo wake ni muhimu pia katika kuipigania Stars ifike nchi ya ahadi.
Hakuna shaka, Kaseja ni moja ya makipa bora kabisa iliyowahi kuwa nao tangu kuundwa kwa Tanzania. Ingawa bado amejiweka kwenye soka la ushindani lakini pia ana vyeti vya ukocha akiwa na umri mdogo vinavyomruhusu kupewa majukumu hayo
. Ujanja na umahiri wake na sasa akiwa na elimu ya ukocha, inaaminika atawaongezea kitu kina Aishi Manula na wenzake kuelekea kwenye vita hii ngumu.
HALI YA TIMU
Kiujumla kikosi cha timu hiyo kinaonekana kuwa na morali kubwa kuelekea mchezo huo kulingana na namna wanavyojifua, matumaini katika nyuso zao na hata lugha ya miili yao inafafanua hilo.
Imeelezwa kuwa tangu kumalizika kwa mechi ya Uganda wachezaji wa Stars wameshakutana kuzungumza pamoja zaidi ya mara tatu, wakijiuliza na kujipanga namna watakavyokwenda kupindua meza ugenini na kuwarejeshea furaha Watanzania.
Ni kama alivyosikika beki wa kutumainiwa wa Stars, Bakari Mwamnyeto hivi karibuni akisema bado kazi haijaisha na wanaamini wao wachezaji ndiyo wenye jukumu kubwa la kuhakikisha wanalisaidia benchi la ufundi kukamilisha mbinu zao uwanjani.
Kauli hiyo inaweza kuwa ndogo lakini ina maana kubwa kuelekea katika mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa mgumu kutokana na upinzani na uwezo wanaokuwa nao Uganda kila wakati wanapoumana na timu za Afrika Mashariki.
MARA YA MWISHO
Mara ya mwisho Stars kutafuta tiketi ya kufuzu kwenye michuano ya Afrika kama ilivyo sasa dhidi ya Uganda ilikuwa mwaka 2019 ikiwania kufuzu Afcon iliyofanyika Cameroon mwaka 2019.
Mpaka mechi ya mwisho katika kundi hilo, Stars haikuwa na uhakika wa kupenya wakati ikikutana na Uganda ambayo ilikuwa imeshafuzu na ilikuwa ikikamilisha tu ratiba na ndipo Stars ikajitutumua na kuifunga mabao 3-0.
Ikafuzu ikimaliza ya pili katika kundi ikiwa na pointi nane dhidi ya Lesotho iliyokuwa na sita na Cape Verde 5, Uganda ikiwa kileleni kwa pointi 13.
Sasa ni mtihani mwingine mbele ya adui yuleyule isipokuwa safari hii Uganda pia inahitaji ushindi ili isonge mbele, yaani nafasi yake ni ushindi dhidi ya Stars hakuna njia nyingine!
Ni kusubiri na kuona nini kitatokea, kama Uganda itakubali kichapo kama ilivyokuwa mara ya mwisho au itapambana kupigania nafasi yake ya Chan mwakani na kufuta historia isijirudie kama ilivyotokea Machi 2019.
BOCCO AONGEZA NGUVU
Nahodha wa Simba, mshambuliaji John Bocco ameongezwa kwenye kikosi hicho kama mkongwe mwenye uzoefu kuelekea katika mchezo huo.
Uwepo wa washambuliaji wengine kama Reliants Lusajo, Danny Lyanga, Kibu Denis, George Mpole na Tepsi Evance inaonesha wazi kwa umri wao katika soka wanahitaji kiongozi kwenye safu yao.
Na Bocco ambaye amekuwa kwenye kiwango cha juu takribani kwa misimu minne mfululizo kabla ya kusumbuliwa na majeraha msimu uliopita, anaonekana anafaa zaidi kwa sasa kututoa hapa tulipo kwa maana ya kutupa mabao.
MAKOCHA WANENA
Kuelekea katika mchezo huo Janza anasema: “Mpira siku hizi hautabiriki sana, unaweza kukuweka juu au chini, niseme dhidi ya Uganda ni hamsini kwa hamsini, vile Uganda iliweza kushinda hapa basi Stars inaweza kufanya hivyo kwao pia.
“Binafsi mimi napenda kushinda na huwa nafurahia kupata ushindi kwa sababu nimewahi kuonja ladha yake na ndiyo maana huwa nafurahia kupata matokeo ya kushinda, tutajaribu kufanya na kuona tunachoweza kukifanya Uganda lakini ushindi ndio tunaoutaka.”
Upande wa Maxime alifafanua kuwa kila kitu kinawezekana kwa ushirikiano na wao kama benchi jipya watapambana kuhakikisha wanaivusha timu hapa ilipo ingawa kazi ya ukocha muda mwingine ni kama kamari unaweza kuona umefanya kila kitu halafu ukashindwa!