Burudani

Msigwa: Litumieni Tamasha la TASUBA kukuza uchumi

BAGAMOYO: Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ni bidhaa ya kiuchumi inayoleta burudani kwa wakazi wa mji huo hovyo walitumie tamasha hilo kama fursa kiuchumi.

Msigwa ameyasema hayo Oktoba 26, 2024 alipokuwa mgeni rasmi wakati wa kilele cha Tamasha hilo lililofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani.

Msigwa amewataka wakazi wa Bagamoyo na maeneo ya jirani kutanua huduma za makazi, chakula, mavazi, malazi, usafiri, bidhaa za kitamaduni na sanaa ili kukidhi mahitaji ya wageni na washiriki wa Tamasha hilo kubwa linalofanyika kila mwaka.

Katika hatua nyingine, Msigwa amesema kuwa Wizara itaongeza bajeti ya Tamasha la 44 mwakani ili kutimiza lengo la kufanyika kwa siku saba huku akiagiza kuwa na wasanii wenye majina makubwa watatumbuiza.

Pia amemuagiza Mkuu wa Chuo hicho kukaa pamoja na wadau ilikuongeza ukubwa na mvuto wa tamasha hilo.

“Nilikuwa hapa mwaka jana Tamasha la 42, niliwaahidi tamasha hili litakuwa bora na mwaka huu tamasha la 43 limekuwa bora, nikushukuru sana Mkuu wa Chuo, lakini pia kazi kubwa inafanywa na Serikali yetu chini ya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kuumarisha nchi na tukifurahia kwa amani ya kutosha, tupo hapa tunafurahi kwa Pamoja, nchi zingine amani hii wanaitafuta”. Amesema Msigwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi hiyo ya TASUBA, Dkt. Herbert Makoye amewashukuru washiriki na wananchi wote waliojitokeza kuhudhuria shughuli hiyo na kuwaahidi kuboresha zaidi katika Tamasha linalofuata la mwakani.

Tamasha hili la Sanaa na Utamaduni, hufanyika kila mwaka katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambapo hukutanisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Tamasha hili hulenga kukuza vipaji, kuuenzi na kuutunza na kurithisha Utamaduni wetu kwa vizazi vijavyo, kutangaza utalii wa mji wa Bagamoyo, pia kutoa ajira kwa wasanii wa nyanja mbalimbali nchini.

Related Articles

Back to top button