Mshambuliaji wa Iran apata Visa ya Marekani, aleta utulivu kambini

SEATTLE, Marekani : Timu ya taifa ya Iran imepata afueni kubwa katika kampeni yake ya Kombe la Dunia baada ya mshambuliaji wake Mehdi Torabi kupewa visa mpya ya kuingia Marekani, hatua itakayomruhusu kuendelea kuichezea nchi yake katika mechi zilizobaki za mashindano hayo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisa mmoja wa timu hiyo Jumanne, Torabi amepewa visa ya kuingia mara nyingi (multiple-entry visa) baada ya juhudi za Shirikisho la Soka la Iran kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA).
Awali, nyota huyo alikuwa amepewa kibali cha kuingia Marekani mara moja pekee, hali iliyozua wasiwasi mkubwa kwa viongozi wa timu hiyo kuhusu uwezo wake wa kurejea nchini humo kwa ajili ya mechi zijazo za Kombe la Dunia.
“Baada ya juhudi za Shirikisho la Soka na uratibu wa FIFA, mchezaji huyo amepewa visa mpya ya kuingia mara nyingi leo,” alisema ofisa huyo wa timu ya Iran.
Aliongeza kuwa kwa visa hiyo mpya, Torabi hatakuwa na changamoto yoyote ya kuambatana na kikosi cha Iran katika mechi zake zijazo na atakuwa huru kusafiri pamoja na timu kwa kipindi chote kilichobaki cha mashindano.
Torabi alikuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwapo kwenye kikosi cha Iran katika mchezo wa kwanza wa Kundi lao uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya New Zealand, ingawa alibaki benchi kwa muda wote wa mchezo huo.
Iran kwa sasa inajiandaa kukabiliana na Ubelgiji katika mchezo muhimu utakaochezwa Jumapili kabla ya kuhitimisha hatua ya makundi kwa kupepetana na Misri jijini Seattle Juni 26.
Changamoto ya visa ni sehemu ya matatizo kadhaa ambayo yameikumba timu ya taifa ya Iran kuelekea na wakati wa mashindano hayo. Ushiriki wa timu hiyo ulitiliwa shaka kufuatia mvutano wa kisiasa uliotokea kati ya Iran, Marekani na Israel katika miezi ya hivi karibuni.
Kutokana na mazingira hayo, mpango wa awali wa kuiweka kambi timu hiyo katika jimbo la Arizona ulifutwa dakika za mwisho na badala yake kikosi hicho kikaweka makazi yake katika mji wa Tijuana nchini Mexico.
Aidha, maofisa wa Marekani walikataa kutoa visa kwa zaidi ya wafanyakazi kadhaa wa timu hiyo, jambo lililowazuia kuambatana na kikosi katika baadhi ya mechi za mashindano.
Kocha wa Iran, Amir Ghalenoei, alilalamikia hali hiyo akisema timu yake ndiyo inayokumbana na changamoto nyingi zaidi katika Kombe la Dunia la mwaka huu. Alidai kuwa wachezaji wake walilazimika kurejea Mexico mara baada ya mchezo wao wa kwanza bila kupata muda wa kutosha wa kupumzika na kujiandaa kwa michezo inayofuata.
Pamoja na vikwazo hivyo, kocha huyo amesema Iran itaendelea kupambana na kufanya kila iwezalo kuhakikisha inafanya vizuri katika mashindano hayo makubwa ya dunia.




