Tennis

Michuano ya tenisi Afrika kufanyika Dar es Salaam

DAR ES SALAAM:TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya tenisi ya vijana wenye umri chini ya miaka 14, yatakayofanyika kuanzia Aprili 6 hadi 13, mwaka huu, katika viwanja vya Gymkhana Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Makamu wa Rais wa Chama cha Tenisi Tanzania (TTA), Rajabu Borry, amesema kuwa Tanzania inajivunia kuwa mwenyeji wa mashindano haya kwa mara ya kwanza katika kundi hili la umri.

Nchi nane za Afrika zitashiriki kwenye mashindano hayo zikiwemo:

Tanzania, Uganda, Kenya, Zimbabwe, Cameroon, Algeria, Afrika Kusini na Nigeria.

Borry amesema kuwa maandalizi yanaendelea vizuri kwa kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), huku akitarajia mashindano haya kuvutia wageni wengi zaidi.

“Tunashukuru Mungu kwa fursa hii, na tunafanya kila jitihada kuhakikisha mashindano yanafanyika kwa mafanikio makubwa,” amesema.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya tenisi kwa vijana, Majuto Majaliwa, amesema kuwa kikosi cha Tanzania kimefanya maandalizi mazuri kupitia mashindano mbalimbali ya mazoezi, jambo linalompa imani kuwa watashiriki kwa ushindani mkubwa.

Naye Kocha Hamis Chande ameeleza kuwa ni heshima kubwa kwa Tanzania kuandaa mashindano haya, kwani mara ya mwisho nchi iliandaa mashindano ya vijana wa umri chini ya miaka 12.

Amepongeza kuwa jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mashindano haya yanafanikiwa na kuiletea Tanzania heshima kimataifa.

Related Articles

Back to top button