Maxime: Hakuna aliye salama ligi kuu

DODOMA: KOCHA Mkuu wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime amesema hakuna aliye salama ligi kuu kuanzia anayeshika nafasi ya sita hadi ya mwisho hivyo, jukumu lao ni kupambana kila mchezo na kushinda.
Dodoma Jiji inatarajia kuikaribisha Fountain Gate kesho kwenye Uwanja wa Jamhuri katika mchezo wa mzunguko wa 21 Ligi Kuu soka Tanzania bara.
Akizungumzia mchezo huo leo Maxime amesema kwa nafasi waliyopo hawana budi kupambana kama fainali kupata pointi tatu zitakazowasogeza mbele.
“Ukitizama msimamo hakuna aliye salama kuanzia nafasi ya sita, kwa maana hiyo na sisi tumo, tunahitaji kumfunga kila mpinzani kujiweka sehemu nzuri. Na mchezo wa kesho ni muhimu kwetu kuhakikisha tunapata matokeo,”amesema.
Maxime amesema kinachowaangusha muda mwingine ni uwepo wa majeruhi kwa nyakati tofauti katika kikosi chake ambapo amekuwa akijaribu kila mara kutengeneza kikosi kulingana na wachezaji waliopo.
Dodoma Jiji iko katika nafasi ya tisa kwa pointi 23 baada ya kucheza michezo 19 na kati ya hiyo, kushinda sita, kupata sare tano na kupoteza michezo nane.
Mwisho