Minziro: Tunawaheshimu Yanga, wasituchukulie poa

MWANZA: KOCHA Mkuu wa Pamba Jiji FC, Fred Felix Minziro, amesema kuwa timu yake inatambua changamoto ya kucheza dhidi ya timu kubwa kama Yanga SC, lakini wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatoa upinzani mkali katika mchezo wao wa leo.
Akizungumza kuelekea pambano hilo litakalochezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza saa 10:00 jioni, Minziro alisema kuwa presha ni jambo la kawaida unapokutana na timu yenye wachezaji bora na uzoefu mkubwa.
“Unapocheza na timu kubwa kama Yanga,ni lazima uwe na mpango mzuri wa mchezo. Tunafikiria jinsi ya kujipanga, kujilinda, na kutafuta mabao. Tumerekebisha makosa yetu katika safu ya ushambuliaji na ulinzi ili kuhakikisha tunatoa ushindani wa hali ya juu,” amesema Minziro.
Pia aliongeza kuwa Pamba Jiji FC imefanya mabadiliko makubwa na mashabiki wanapaswa kutegemea mchezo mzuri wenye ushindani.
“Tunawaheshimu Yanga kwa sababu wamewekeza vizuri, lakini sisi pia tumeimarika. Mashabiki wategemee kuona mechi kali na yenye ushindani,” ameongeza.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na mvuto mkubwa, kwani Pamba Jiji FC itakuwa na faida ya kucheza nyumbani mbele ya mashabiki wao, huku Yanga ikisaka pointi muhimu ili kuendelea kuimarisha nafasi yake kwenye ligi.