Materazzi: Kifo cha De Miguel kimenikumbusha nilivyopigwa kichwa na Zidane

ITALIA: ALIYEKUWA beki wa timu ya taifa ya Italia, Marco Materazzi, amesema kifo cha mshambuliaji wa Hispania, Jesus de Miguel, kufuatia kugongana uwanjani kimemfanya kutafakari upya tukio la mwaka 2006 ambapo nyota wa Ufaransa, Zinedine Zidane, alimpiga kwa kichwa katika fainali ya Kombe la Dunia.
Materazzi amesema kifo cha De Miguel, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 30 baada ya kupata mshtuko wa moyo kufuatia kugongana na kipa Jesus Owono wa FC Andorra katika mchezo wa Ligi Daraja la Pili Hispania, kimemfanya kumshukuru Mungu kwa kuwa hakupata madhara makubwa wakati wa tukio lake na Zidane.
Tukio hilo lililotokea katika fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani lilisababisha Zidane, aliyekuwa nahodha wa Ufaransa, kupewa kadi nyekundu baada ya kumpiga Materazzi kifuani kwa kichwa. Italia iliibuka bingwa kwa ushindi wa penalti.

Akizungumza na chombo cha habari cha La Gazzetta dello Sport, Materazzi alisema tukio hilo bado linamkumbusha mambo mengi hata baada ya kupita miaka 20.
Alisema kifo cha De Miguel kimemfanya kutambua umuhimu wa maisha na kushukuru kuwa hakupatwa na madhara makubwa katika tukio hilo.
Materazzi pia alifichua kuwa alikutana na Zidane mwaka 2010 kabla ya mchezo mmoja, ambapo alimkaribia na kumsalimia licha ya historia yao ya kutofautiana. Kwa mujibu wake, Zidane alimwambia kuwa yaliyotokea yalikuwa yamepita na mambo kama hayo hutokea katika soka.
Hata hivyo, Materazzi alisema alisikitishwa baadaye baada ya Zidane kukanusha kuhusu mkutano huo, akidai kuwa alifikiri Materazzi alikuwa shabiki aliyekuja kumsalimia.




