Mastaa wa muziki Nigeria kukutanishwa ulingoni

LAGOS: MASTAA wa muziki nchini Nigeria Portable na Speed Darlington wanatarajiwa kumaliza ugomvi wao katika mitandao ya kijamii katika pambano la ndondi la watu mashuhuri.
Pambano hilo litafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Balmoral nchini Nigeria mnamo Aprili 18 likijumuisha mabondia mbalimbali kutoka Mataifa sita, Ikiwemo Ghana, Tanzania, Nigeria, Uingereza na Italia na Misri.
Pambano la ngumi la wawili hao linatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa utakaowahusisha mashabiki wao kwani wasanii hao wote wanatamani kudhihirisha uwezo wao wa kurusha ngumi ulingoni baada ya kutupiana maneno mtandaoni kwa muda mrefu.
Wanamuziki hao wawili wamekuwa wakichuana vikali mtandaoni, na mechi hii inatoa fursa kwao kusuluhisha tofauti zao kwa njia ya kipekee na ya kusisimua lakini pia watakuwa wanachangia jamii inayowazunguka kwa sababu asilimia kubwa ya pato la pambano hilo inaelekezwa kwa jamii.
“Kwa kuhudhuria pambano hilo watazamaji hawatashuhudia tu mchezo wa ndondi wenye kusisimua lakini pia watachangia kuleta mabadiliko chanya na kuunga mkono mambo yanayofaa.
“Pamoja na dhamira yake ya ujenzi wa jamii, imewekwa kuleta athari ya kudumu kwa maisha ya watu binafsi na familia zinazohitaji msaada.”