BFT yawafunda waamuzi, majaji Mwanza
MWANZA: Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) limewafunda walimu, waamuzi na majaji jijini Mwanza ikiwa ni mipango waliyojowekea katika kuendeleza mchezo huo nchini.
Akizungumzia mafunzo hao Rais wa BFT Lukelo Willilo amesema utoaji wa mafunzo hao ni mwendelezo kwani walishatoa awamu ya kwanza Dar es Salaam na wataendelea kuhakikisha mchezo huo unachezwa kila mahali.
“Tunaendelea kutekeleza kwa vitendo tuliyoyaahidi kwa kuwekeza zaidi katika mafunzo ya Kitaifa na Kimataifa ya walimu, waamuzi na majaji na wasimamiaji wa mchezo na baadae tutawafikia na viongozi wa vyama vya mikoa na wilaya” amesema.
Kwa mujibu wa Willilo, wanatarajia kuendesha mafunzo mengine ya awali kwa walimu, waamuzi, majaji na wasimamiaji wa mchezo wa ngumi Novemba 2024 na kuandaa mashindano ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere mwezi wa April, 2025.
Mara ni Mkoa wenye historia kubwa katika mchezo wa Ngumi katika Taifa ikiwatoa wanamasumbwi bora na mahiri walioiletea sifa Taifa Kimataifa katika mchezo wa Ngumi katika nyakati tofauti.
Moja ya wanamasumbwi hao ni Mabingwa wa Afrika William Isangura na ndugu yake Makoye Isangura. Wengine ni Nassoro Michael, Michael Changalawe, Juma Bugingo “Mkono wa Spring”, Rajabu Hussein, Marehemu Joseph Magesa, Samwel Changarawe, Clement na Ezra Mtolela.
Katika wanamasumbwi wa kizazi kipya ni Bingwa wa misimu yote na Nahodha wa timu ya Taifa “Faru Weusi wa Ngorongoro” Yusuf Changalawe ambaye ni Mshindi wa medali za Shaba katika michezo ya Jumuiya ya Madola Birmingham 2022, Ubingwa wa Afrika Yaounde 2023 na Mashindano ya Africa Accra 2024. Pia yupo Musa Wambura Maregesi ambaye ni mshindi wa medali ya shaba Michezo ya Africa Accra 2023.