Mario Rivera aitamani fainali Cecafa

DAR ES SALAAM: KOCHA wa timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes), Mario Rivera, amesema wachezaji wake wana hamu na ari kubwa ya kufanya vizuri katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Burundi leo, huku wakilenga kufika fainali na pia kupata nafasi ya kufuzu fainali za AFCON U20.
Rivera amesema maandalizi ya timu yanaendelea vizuri, akieleza kuwa wachezaji wameonesha utayari mkubwa na wanataka kuthibitisha uwezo wao katika mchezo huo muhimu.
“Tunaiandaa timu, na wachezaji wana hamu kubwa pamoja na shauku ya kufikia malengo yetu, ikiwamo kupata moja ya nafasi za kufuzu AFCON na, bila shaka, kufika fainali ya CECAFA.

Kocha huyo amesema kiwango kilichooneshwa na vijana wake katika michezo iliyopita kimempa matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo huo wa nusu fainali, akiwataka wachezaji kuendelea kuwa na nidhamu na kujituma.
Aidha, Rivera amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani kesho kuiunga mkono Ngorongoro Heroes, akisema uwepo wa mashabiki utawapa nguvu zaidi wachezaji katika mchezo huo muhimu.
Ngorongoro Heroes itakutana na Burundi katika mchezo huo wa nusu fainali ya michuano ya kufuzu AFCON U20 Kanda ya CECAFA, ikiwa na lengo la kusonga mbele hatua ya fainali na kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu fainali za AFCON U20.
Tanzania imetoka kundi A ikiongoza kwa pointi sita baada ya kuzifunga Rwanda na Ethiopia huku Burundi ikitoka kuongoza kundi C baada ya kuzifunga Kenya na Sudan Kusini.




