Mandonga aapa kuua mtu leo

ZANZIBAR; “NITAKUUA rafiki yangu,” ni kauli ya bondia Mtanzania Karim Mandonga kwa mpinzani wake kutoka Canada, Michael Williams, saa chache kabla ya kupanda ulingoni usiku wa leo Zanzibar.
Mandonga ametoa kauli hiyo katika mazungumzo yake na Williams, akimweleza mpinzani wake kuwa wahakikishe wanakutana ulingoni leo, huku akionesha kujiamini kabla ya pambano hilo.
“Nitakuua rafiki yangu. Usijali, tuone kama unaweza kubaki uwanjani. Hakikisha unafika
Leo… hakuna tatizo, tutaonana,” amesema Mandonga katika ujumbe wake kwa Williams.
Kauli hiyo imeongeza hamasa miongoni mwa mashabiki wanaosubiri kuona kitakachotokea ulingoni, hasa kutokana na mtindo wa Mandonga kutumia kauli za aina hiyo kabla ya mapambano yake.
Mandonga na Williams wanatarajiwa kukutana katika pambano la ngumi litakalofanyika Zanzibar usiku wa leo, huku kila mmoja akilenga kutumia uwezo wake kupata ushindi mbele ya mashabiki.
Pambano kuu la usiku huo litawakutanisha bondia kutoka Malawi, Hary Mkacha, dhidi ya Mtanzania Hamis Magazeti, katika pambano jingine linalotarajiwa kuwa kivutio kwa mashabiki wa ngumi.




