Ndumbaro kushuhudia Tag la Mama Samia
DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, DK. Damas Ndumbaro, anatarajiwa kuwa mgeni akishuhudia mabondia 12 kwenye pambano la ‘Dar Boxing Derby’, linalotarajiwa kufanyika Juni 29, mwaka huu, Viwanja vya Posta Kijitonyama, jijini hapa.
Akizungumza na Mratibu wa pambano hilo, Seleman Semenyu amesema Ndumbaro atakuwa mgeni rasmi katika pambano hilo waliloipa jina la ‘TAGI LA MAMA SAMIA’, hiyo ni baada ya Rais, Samia Suluhu Hassan kuwa na mchango mkubwa katika sekta ya Michezo.
Amesema mandalizi yanaendelea vizuri katika pambano hilo ‘Main Card’, atakuwa Ramadhani Nassib dhidi ya Juma Choki, watacheza uzani wa 59 Kg la raundi 8, ikiwa ni mara ya kwanza mabondia hao kukutana kila mmoja akiwa na rekodi nzuri katika mchezo huo.
“Kila kitu kipo sawa, mabondia wapo kambini wanajiandaa, tunaimani itakuwa pambano nzuri na kuvutia wapenzi wa mchezo huu kwa sababu kuna Nassib na Choki ni mara ya kwanza kukutana na wote mabondia wazuri,” amesema Semunyu.
Mabondia wanaosindikiza pambano hilo ni Tonny Rashid dhidi ya Oscar Richard uzani wa 84Kg, Saidi Mkola dhidi ya Saidi Bwanga uzito wa 58Kg, Loren Japhet atazichapa na Issa Nampepeche, Charles Tondo atapanda ulingoni dhidi ya Haidary Mchanjo, Kassim Hamad dhidi ya Gabriel Moris.
Ramadhani Bonny atapanda ulingoni dhidi ya Adam Ngange, Gabriel Chola atanyukana na Frank Nampumula, Fred Sebastian dhidi ya Barnaba Alexender, Shazi Hija na Ibada Jafary na Peter Damian na Rajab Chanda kwa wanawake Najma Isike dhidi ya Nasra Msimi katika uzito wa 61 kg raundi ya sita.