Masumbwi

Dubois bado anamtaka Usyk ulingoni

LONDON: BINGWA wa Dunia wa WBO, Daniel Dubois ‘The Dynamite’ anataka kupigana na Oleksandr Usyk kwa mara ya tatu, akiamini sasa yuko fiti kumdunda.

Dubois raia wa Uingereza alitoa tamko hilo baada ya ushindi wake dhidi ya Fabio Wardley aliyemtwanga K.O katika raundi ya pili ya pambano hilo lililopigwa Ukumbi wa O2 Arena.

“Fabio ana uwezo mkubwa wa kuhimili vipigo. Anajulikana kwa kuvumilia mashambulizi makali, lakini nilikuwa nikimzidi nguvu. Ilinibidi tu nitulie kidogo na kujipanga upya. Nataka kujua nani anayefuata!

“Nikipewa pambano kwa mara ya tatu kucheza na Oleksandar Usyk, naweza kumpiga, kwa sasa nipo tayari kwa pambano la tatu.

“Bila shaka, ningependa sana hilo, safari hii tutashinda. Tumerekebisha makosa yetu na sasa tuko tayari kushinda,” alisisitiza Dubois.

Tayari Dubois alishapigana na Usyk kutoka Ukraine mara mbili, na mara zote Usyk ambaye hajawahi kushindwa na amewahi kuwa bingwa asiyepingwa wa uzito wa juu mara mbili, alimshinda Dubois.

Agosti, 2023 Usyk alimchapa Dubois kwenye pambano la kwanza katika raundi ya tisa. Waliporudiana Uwanja wa Wembley mnamo Septemba, mwaka jana, Usyk akampiga K.O Dubois kwenye raundi ya tano.

Aidha, Usyk aliachia mataji yote ya dunia aliyokuwa nayo, hatua iliyomwezesha Dubois kutwaa mkanda wa WBO kabla ya pambano lake la kwanza dhidi ya Wardley, Filip Hrgovic kuchukua mkanda wa IBF akimchapa Moses Itauma, na Agit Kabayel kupandishwa hadhi kuwa bingwa wa dunia wa uzito wa juu wa WBC.

Related Articles

Back to top button