Makonda aibua maswali 22 mkataba wa jezi ya Taifa

DAR ES SALAAM:WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Paul Makonda ameibua maswali 22 kuhusu mkataba wa jezi ya Taifa Stars, akisema kuna haja ya kupitia nyaraka za makubaliano hayo ili kupata majibu kuhusu thamani, ubora, matumizi ya nembo na haki za kibiashara zilizotolewa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Dar es Salaam Leo Makonda amesema suala la jezi ya Taifa si jambo la mtu binafsi, bali ni alama ya utambulisho wa nchi, hivyo Serikali inapaswa kuhakikisha bidhaa hiyo ina ubora, inapatikana kwa wananchi na inatumika kuitangaza Tanzania.
Waziri amesema katika kuupitia mkataba huo ameona una vipengele vinavyohusisha udhamini na usambazaji wa vifaa, huku akitaka majukumu ya kila upande yawekwe wazi.
Amesema mkataba unaweka ada ya udhamini ya Sh1.5 bilioni kwa miaka mitano pamoja na vifaa vya timu za Taifa vyenye thamani ya Sh300 milioni kwa mwaka, lakini amehoji namna thamani hiyo ilivyofikiwa.
“Swali nililojiuliza ni kwamba tulifikaje kwenye Sh1.5 bilioni? Haki zote za biashara zinazotolewa kwa miaka mitano zilifanyiwa valuation gani?” amehoji.
Amesema mkataba pia una kipengele cha kufanya mapitio ya utekelezaji kila mwaka, hivyo anataka mapitio hayo yafanyike ili kuangalia kama thamani na masharti yaliyowekwa bado yanaendana na mwenendo wa timu za Taifa.
Waziri amesema pia ameibua suala la VAT, akitaka kuwekwa wazi nani anabeba gharama hiyo na utaratibu gani unatakiwa kutumika iwapo thamani ya malipo inabadilika.
Amehoji pia kuhusu ‘requirement specification’ ya jezi hiyo, akitaka kujua vigezo vilivyowekwa kuhusu ubora wa jezi, nani aliyepima na nani aliyethibitisha kuwa bidhaa iliyotolewa imekidhi viwango vilivyokubaliwa.
“Specification hiyo iko wapi? Jezi inatakiwa kuwa na kigezo au kiwango gani? Nani alipima? Nani alithibitisha kwamba imekidhi specification?” amehoji.
Amesema majibu ya maswali hayo yanapaswa kupatikana kwenye nyaraka za mkataba na utekelezaji wake, badala ya mjadala kuishia kwenye maoni ya watu kuhusu jezi hiyo.
Waziri amesema pia kuna haja ya kuangalia bei ya jezi ili iweze kufikiwa na mashabiki wengi, akisema kila shabiki anapaswa kupata nafasi ya kununua na kuvaa jezi ya Taifa.
Amesema jezi hiyo inapaswa kuonekana kama bidhaa ya Taifa na si bidhaa ya kawaida ya klabu.
Amesema Serikali inataka kuona jezi hiyo ikipata soko nje ya Tanzania na kuwa sehemu ya kuitangaza nchi duniani, akitoa mfano wa uwezekano wa kukutana na jezi ya Tanzania katika maduka ya Nike yaliyopo katika nchi mbalimbali.
Amesema endapo mfumo huo utawekwa vizuri, Tanzania inaweza kupata manufaa ya kibiashara huku jezi hiyo ikiendelea kuitangaza nchi katika masoko ya kimataifa.
Aidha, amesema kuna umuhimu wa kuwapa nafasi vijana wenye vipaji vya ubunifu kubuni jezi za Taifa, ili bidhaa hiyo iweze kuakisi utambulisho na ubunifu wa Watanzania na Afrika.
Amesema mjadala kuhusu jezi haupaswi kulenga kumtafuta au kumlaumu mtu, bali kuhakikisha Tanzania inapata bidhaa bora na makubaliano yenye manufaa kwa Taifa.
Waziri amesisitiza kuwa Serikali na wadau wa michezo wanapaswa kushirikiana katika kutengeneza mpango wa kuitumia jezi ya Taifa kuongeza thamani ya Taifa, huku akisema ukosoaji na ushauri vinapaswa kutumiwa kuboresha bidhaa hiyo.
Amesema mwisho wa mchakato huo ni kupata jezi yenye ubora, inayopendwa na mashabiki, inayoweza kununuliwa kwa urahisi na inayoweza kuitangaza Tanzania ndani na nje ya nchi.




