DAR ES SALAAM: KLABU ya Yanga inaendelea kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao ili kufikia malengo ya msimu ujao.
Taarifa zinaeleza kuwa klabu hiyo imekamilisha mazungumzo na winga wa Ihefu FC, Manu Bola ambaye anatarajia kutua nchini wiki ijayo kwa ajili ya kusaini mkataba kutumikia timu hiyo.
Yanga imedhamiria kuimarisha kikosi cha timu hiyo kwa kufuata mapendekezo ya benchi lao la ufundi chini ya Kocha wao Mkuu, Miguel Gamond akihitaji kuimarisha timu yake kuhakikisha msimu ujao wanafanya kweli hasa michuano ya Kimataifa.
Gamondi anataka kuitengeneza timu ambayo inaweza kufika nusu fainali au fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo msimu uliopita waliishia hatua ya robo fainali akiamini Bola anaweza kuwa msaada kwao.
Bola anatarajiwa kutengeneza kombinesheni imara na wachezaji wapya wanaosajiliwa na wanaosalia akiwemo Stephan Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Max Nzengele na Mudathir Yahya.
Yanga ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2023/24 wataipeperusha bendera ya Tanzania katika michuano hiyo Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo wamedhamiria kufanya kweli na kufika hatua za juu tofauti na msimu uliopita.
Kwa mujibu wa Chanzo chetu kilicholifikia SpotiLeo ni kuwa Bola na Yanga kila kitu kimeenda vizuri kwani pande zote mbili zimekubaliana na sasa kilichosalia ni kusaini mkataba na kuanza kuitumikia klabu hiyo.
“Mazungumzo kati ya nyota huyo na Yanga yamekamilika, na hivyo kuanzia Jumatatu ya wiki ijayo anatarajiwa kutua nchini kwa ajili ya kusaini mkataba, kuwa sehemu ya kikosi cha mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara,” kilisema chanzo hicho.
Kwa upande wake Afisa habari wa Yanga, Ali Kamwe licha ya kutokuwa wazi wachezaji ambao wanasajiliwa, alisema watafanya usajili wa kishindo katika dirisha hili kubwa la usajili kutokana na mapendekezo ya Kocha Gamondi.
“Kama msimu ujao watu walifungwa bao 7 katika Michezo miwili safari hii wajipanga sana, usajili unaofanywa ni mzuri, kila kitu kipo kwenye mpango kazi na malengo yetu ni kuona tunakuwa imara kuelekea msimu mpya,” amesema Kamwe huku akirusha dongo kwa Simba ambao waliwafunga jumla ya mabao 7-2 michezo yote miwili msimu uliopita.