Eve atwaa taji la Miss Afrika International 2026

DAR ES SALAAM: BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limempongeza Mtanzania Eve Godwin kwa kutwaa taji la Miss Africa International 2026.
Ushindi huo ni kielelezo cha kuitangaza Tanzania katika majukwaa ya kimataifa ya urembo.
Basata imeeleza kuwa mafanikio hayo ni kielelezo cha uwezo, vipaji na ubora walionao Watanzania katika kushiriki na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.
Aidha, Baraza hilo limeeleza kuwa ushindi huo ni fahari kwa Taifa na unaendeleza mwendelezo wa mafanikio pamoja na uwakilishi mzuri wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa ya urembo.
Katika hatua nyingine, Basata limewapongeza wadau mbalimbali wanaoendelea kutoa mchango wao katika kuunga mkono, kuhamasisha na kukuza vipaji vya Watanzania vinavyojitokeza katika majukwaa mbalimbali.
Limesisitiza kuwa ushirikiano wa wadau ni muhimu katika kukuza sanaa, kuinua vipaji na kuitangaza Tanzania katika medani za kimataifa.
Basata limewahimiza Watanzania kuendelea kuunga mkono vipaji vya ndani ili kuhakikisha nchi inaendelea kung’ara na kujivunia mafanikio ya vijana wake katika majukwaa mbalimbali duniani.




