Rosemary Uisso aingia Top 10 Miss global 2026

TANZANIA imeendelea kung’ara katika jukwaa la kimataifa la urembo baada ya mwakilishi wake katika mashindano ya Miss Global 2026, Rosemary Uisso maarufu kama KYM, kutwaa tuzo ya Best National Costume, inayotambua vazi bora la kitaifa.
Ushindi huo ni hatua muhimu kwa Tanzania katika mashindano hayo, ambapo Rosemary ameonyesha utajiri wa utamaduni, sanaa na ubunifu wa mavazi ya asili yanayoitambulisha nchi katika medani ya kimataifa.
Mbali na kutwaa tuzo hiyo, Rosemary ameendelea kufanya vizuri katika mashindano hayo baada ya kufanikiwa kuingia hatua ya washiriki 25 bora (Top 25) na baadaye kusonga mbele hadi hatua ya washiriki 10 bora (Top 10).
Mafanikio hayo yameongeza matumaini kwa mashabiki wa urembo nchini wanaofuatilia safari yake katika mashindano hayo, huku akipewa pongezi kwa kuendelea kuiwakilisha Tanzania katika jukwaa hilo.
Tuzo ya Best National Costume inaipa nafasi Tanzania kuonyesha utambulisho wake kupitia mavazi yanayoakisi urithi wa kitamaduni, huku ikidhihirisha nafasi ya sanaa na ubunifu katika kuitangaza nchi kimataifa.
Kupitia mafanikio hayo, Rosemary ameendelea kuwa sehemu ya juhudi za kuitangaza Tanzania nje ya mipaka yake, akiwakilisha utamaduni na ubunifu wa Watanzania mbele ya washiriki kutoka mataifa mbalimbali.
Mashabiki na wadau wa urembo wamehimizwa kuendelea kumpa hamasa na kumuunga mkono Rosemary anapoendelea na safari yake katika mashindano hayo, wakitumaini kuona akipiga hatua zaidi.
Kwa sasa, macho ya Watanzania yanaendelea kuelekezwa kwa KYM, ambaye mafanikio yake katika Miss Global 2026 yameongeza hamasa na fahari ya kuona utamaduni wa Tanzania ukipata nafasi ya kutambulika kimataifa.



