Burudani

Mafunzo ya Urembo Kuwanufaisha Wanawake 1,000

DAR ES SALAAM:KAMPUNI ya Maybelline New York imetangaza programu ya mafunzo kwa wanawake 1,000 wa Tanzania katika sanaa ya urembo wa kitaalamu, mafunzo yanayotarajiwa kuanza ndani ya miezi mitatu ijayo.

Kutangazwa kwa mpango huu kumeenda sanjari na kuingia rasmi kwa bidhaa za urembo zinazozalishwa na Maybelline katika soko la Tanzania, huku ukilenga kuwapa wanawake ujuzi utakaofungua milango ya ajira na ujasiriamali katika sekta ya urembo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa bidhaa hizo, Victoria Karanja, Meneja Mkuu wa Bidhaa za Watumiaji wa kampuni hiyo, amesema kuwa Maybelline New York ni zaidi ya vipodozi, na pia ni chachu ya mapinduzi ya kiuchumi kwa wanawake na wasichana wa Tanzania.

“Kuingia kwetu Tanzania ni hatua ya kujenga uwezo wa kujiamini, ubunifu, na kujieleza. Lengo letu ni kuwawezesha wanawake, siyo tu kwa kununua na kutumia bidhaa za urembo, bali pia kwa kuwapa ujuzi utakaowawezesha kubadilisha maisha yao kiuchumi,” amesema.

Amesema programu hiyo inatarajiwa kuleta fursa mpya za kiuchumi kwa kuwawezesha wanawake kuanzisha biashara zao wenyewe au kupata ajira katika saluni, maduka ya urembo na sekta ya burudani.

“Kwa kujifunza mbinu za urembo wa kitaalamu, washiriki hawataongeza tu uwezo wao wa kupata kipato, bali pia watachangia ukuaji wa sekta ya urembo nchini Tanzania,” ameongeza.

Karanja amesema kuwa mafunzo hayo yataendeshwa na wasanii wa urembo wenye majina makubwa kutoka ndani na nje ya nchi, ambao watawafundisha washiriki mbinu za hali ya juu, mikakati ya biashara, na ujuzi wa bidhaa ili kuwasaidia kujenga taaluma zenye mafanikio.

Related Articles

Back to top button