La La, Carmelo wakamilisha mchakato wa talaka

NEW YORK: MWIGIZAJI, La La Anthony na Carmelo Anthony wameelezwa kufikia makubaliano katika mchakato wao wa talaka, akisubiriwa hakimu kuidhinisha suala hilo.
Kulingana na nyaraka za mahakama zilizopatikana na Mtandao wa TMZ, Carmelo ambaye ni gwiji wa NBA aliiarifu mahakama wiki hii kuhusu makubaliano hayo.
Aidha, awali La La aliwasilisha ombi la talaka mwaka 2021, akitaja sababu ya kutoelewana kusikoweza kutatuliwa.
Wawili hao walitengana mwaka 2017 baada ya miaka saba ya ndoa, baada ya uvumi kwamba Melo alimsaliti La La. Walijaribu kurekebisha mambo, lakini hatimaye wakaamua kuachana.
Wakati wa uwasilishaji wa ombi la talaka, wawili hao walikuwa wametengana kwa muda, lakini waliendelea kuwa marafiki.
Na sasa talaka hiyo imekamilika baada ya mtoto wao wa kiume, Kiyan, mwenye umri wa miaka 19, kufikia utu uzima, jambo linalofanya suala la matunzo ya mtoto kutokuwa na umuhimu tena.
Kiyan ndiyo kwanza ameanza safari yake ya mpira wa kikapu katika ngazi ya chuo, akiwa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Syracuse, mahali ambapo Melo aliwahi kucheza na kushinda Ubingwa wa Kitaifa.
Hata hivyo, Melo ana mtoto mwingine wa kike, Genesis aliyezaa na Mia Burks mwaka 2017. Uhusiano huo unatajwa kama chanzo cha mtafaruku wa ndoa ya Melo ingawa Melo na Mia pia hawapo pamoja kwa sasa.




