Drake akanusha kumpa mimba Keshia Chante

NEW YORK: WAWAKILISHI wa rapa Drake wamekanusha vikali uvumi kwamba rapa huyo anatarajia mtoto na mwimbaji na mtunzi, Keshia Chante, zaidi wakisema taarifa hizo ni upuuzi mtupu.
Iko hivi, Keshia alitangaza habari za ujauzito wake jana Jumanne kupitia makala ya Jarida la Hello! Akionekana mwenye furaha na kung’aa katika picha za ujauzito huku akifichua anatarajia mtoto wa kiume.
Keshia hakutaja nani baba wa mtoto huyo, japo alidokeza kwenye mitandao ya kijamii kuwa baba huyo anahusika na tasnia ya muziki, ambapo haikuchukua muda, jina la Drake likahusishwa vikali na suala hilo.
Keshia, raia wa Canada ana urafiki na Drake na watu waliharakisha kuhitimisha mambo, wakidai ukaribu wao haukuwa wa kawaida katika siku za hivi karibuni.
Sasa, Kampuni ya The Agency Group, ambao husimamia mawasiliano ya dharura na mahusiano ya umma ya hadhi ya juu kwa ajili ya Drake, wamekanusha bila shaka yoyote uvumi huo wakidai hauna ukweli wowote.
Kama inavyofahamika, mpaka sasa Drake ni baba wa mtoto mmoja, Adonis, 9 aliyezaa na Sophie Brussaux, ambaye alifunga ndoa hivi karibuni kwenye msimu wa joto uliopita.
Kwa kawaida Drake huweka maisha yake ya kimapenzi kuwa ya siri, ingawa hivi karibuni kulizuka uvumi wa uhusiano wa kimapenzi kati yake na mwanamitindo, Pinkchyu.




