Kocha Azam FC alia na ratiba Ligi Kuu
DAR ES SALAAM: WAKATI Kocha wa Azam FC, Rachid Taoussi akilia na ratiba, mpinzani wake wa Coastal Union, anahitaji pointi muhimu kutoka kwa wanalambalamba hao kwenye mchezo wa kesho wa Ligi Kuu Bara.
Azam FC wametoka kucheza mechi ya ligi Alhamisi Septemba 19, wakiwa ugenini na KMC FC na kesho wanashuka dimbani wakiwakaribisha Coastal Union Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi.
Kocha wa Azam FC, amesema ratiba haikuwa rafiki baada ya kila siku mbili wanacheza mechi hali ya kuwa anatakiwa kuwa makini kulingana na kuwapa nafasi wachezaji wake kucheza.
Amesema ameandaa vizuri kikosi chake na wachezaji wapo tayari kwa ajili ya kutafuta pointi tatu katika mchezo wa kesho dhidi ya Coastal Union.
“Baada ya ushindi dhidi ya KMC tulianza kuandaa timu kwa ajili ya mchezo na Coastal Union, wachezaji ni watoto wangu nazungumza nao, licha ya kuwaanda kiufundi lakini kisaikolojia kwa kuwaambia zawadi nzuri ni kutafuta ushindi kila mechi,” amesema Taoussi
Naye kocha wa Coastal Union, Joseph Lazaro amesema wamedhamiria kufuta yale ambayo yaliyojitokeza mechi za nyuma na kupoteza mechi ya nyumbani na wanaenda kutafuta pointi tatu katika mchezo wa kesho dhidi ya Azam FC.
“Tumesahihisha makosa yaliyojitokeza mechi iliyopita ikiwa sehemu ya ulinzi kuhakikisha tunazuia na kufanya mashambulizi, mabadiliko yatatokea kwenye safu ya ulinzi,” amesema Kocha wa Coastal Union.