Kikapu

Knicks watinga Fainali za NBA kwa mara ya kwanza tangu 1999

NEW YORK: TIMU ya New York Knicks ya Marekani imefuzu kucheza Fainali za Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA) kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1999 baada ya kuichapa Cleveland Cavaliers kwa pointi 130-93 katika mchezo wa nne wa fainali za Ukanda wa Mashariki uliochezwa mjini Cleveland.

Ushindi huo umeifanya Knicks kumaliza kwa ushindi wa michezo minne mfululizo (4-0) na kuweka rekodi ya ushindi wa michezo 11 katika hatua ya mtoano ya msimu huu.

Nyota wa Knicks, Karl-Anthony Towns, aliongoza kwa kufunga pointi 19 na kudaka rebounds 14 huku OG Anunoby akiongeza pointi 17. Landry Shamet alitokea benchi na kufunga pointi 16 baada ya kupachika mashuti manne ya pointi tatu.

Pia Jalen Brunson na Mikal Bridges walifunga pointi 15 kila mmoja huku Josh Hart akichangia pointi sita, rebounds 11 na pasi sita za mabao.

Brunson alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mfululizo huo baada ya kuwa na wastani wa pointi 25.5 na pasi za mabao 7.8 kwa kila mchezo.

Kwa upande wa Cavaliers, Donovan Mitchell alifunga pointi 31 huku Evan Mobley akiongeza pointi 15 na rebounds saba.

Knicks walitawala mchezo huo tangu robo ya kwanza baada ya kufanya mfululizo wa pointi 20 bila majibu na kufungua pengo kubwa lililowapa nafasi ya kuongoza hadi mwisho wa mchezo.

Kocha wa Cavaliers, Kenny Atkinson, amesema Knicks walicheza kwa kiwango kikubwa na kustahili ushindi huo.

Kwa ushindi huo, Knicks sasa wanasubiri mshindi wa fainali za Ukanda wa Magharibi ili kucheza Fainali za NBA wakisaka taji lao la kwanza katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili.

Related Articles

Back to top button