Kizz Daniel atambulisha mbili kusherehekea miaka 10 ya muziki na mafanikio yake
NIGERIA: MKALI wa Afrobeats, Kizz Daniel anaendelea kusherehekea muongo mmoja wa ubora wa muziki wake huku akiachia nyimbo mbili ukiwemo ‘Marhaba’ na ‘We Must’.
Nyimbo hizo mpya ni sehemu ya sherehe zinazoendelea ya kuadhimisha miaka yake ya ‘Vado At 10’, miaka kumi ya muziki wake, kutambulika duniani kote, na uungwaji mkono anaopata kutoka kwa mashabiki.
‘Marhaba’, iliyotayarishwa na dyad, Ramii na Suhel Nafar, imechangawa na sauti ya Kizz Daniel na beats mpya yenye mchanganyiko wa vionjo Afrobeats na muziki wa kitamaduni wa Kaskazini mwa Afrika.
Neno la Kiarabu ‘Marhaba,’ alilotumia msanii huyo tafsiri yake ni ‘Welcome/hello’ kwa Kiingereza, ni mojawapo ya semi zinazotumiwa sana Kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati.
Kizz Daniel alisema ametumia neno hilo kama kuleta ushawishi mkubwa kwa watu wa mataifa mengi duniani kote kwa sababu neno Marhaba linatumika sehemu kubwa ya dunia.
Akizungumzia wimbo wa ‘We Must’, uliotayarishwa na Ayzed, Kizz amesema wimbo huo unazungumzia uthabiti na dhamira. Nguvu ya mdundo ya wimbo na mashairi ya kutia moyo yanaufanya kuwa wakati wa kipekee katika sherehe za kumbukumbu ya miaka yake 10 ya Kizz Daniel, na kukamata kiini cha safari yake ya muongo mmoja katika tasnia ya muziki.
Awali wimbo huu alipanga kumshirikisha rapa kutoka nchini Uingereza lakini alichelewa kupokea wimbo huo kwa ajili ya kuweka sauti yake hivyo Kizz aliamua kuuimba mwenyewe na kuongeza vionjo vyake hadi ukakamilika na akaamua kubadili jina na kuuita ‘We Must’.