Ligi Daraja La Kwanza

Kifaru: Tumekuja kutalii Championship

MOROGORO: Klabu ya Mtibwa Sugar imesema imekwenda kwenye Ligi ya Championship kwa ajili ya kutalii lengo lao ni kujifunza na kupambana kurudi Ligi Kuu na somo kwa klabu nyingine.

Mtibwa Sugar ilishuka daraja msimu uliopita na mwaka huu inashiriki Ligi ya Championship kujaribu bahati yao ya kurejea kunako Ligi Kuu.

Akizungumza na SpotiLeo Leo Msemaji wa Mtibwa Sugar Thobias Kifaru amesema kushuka kwao na kucheza Ligi hiyo ni kama wamekwenda kufanya utalii ili hatimaye wapambane na kurejea tena wanakostahili.

“Huku tumekuja kutembea naamini tutajifunza changamoto zilizopo ili hapo baadaye tukipanda turudi na somo la kuzipa klabu zilizoko juu ndo maana nasema tumekuja kutalii,”amesema.

Amesema anajua ligi hiyo ni ngumu kwasababu kuna timu nyingi ziliwahi kushuka na kupotea kabisa lakini wao wamejipanga vizuri wasije wakapotea kana wenzao.

Mtibwa tayari imeanza kampeni ya kupanda Ligi Kuu vizuri baada ya mchezo wa kwanza kushinda dhidi ya Green Warriors mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Manungu Turiani.

Kesho watacheza dhidi ya Cosmo Politan kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro. Timu hii mchezo uliopita imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya African Sport.

 

Related Articles

Back to top button