Uhuru Seleman aomba kukutana na Waziri Makonda

DAR ES SALAAM: Mchezaji wa zamani wa Simba na kocha wa viungo wa Klabu ya KMC, Uhuru Seleman, amesema anatamani kupata nafasi ya kukutana na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda, akiamini anaweza kumsaidia kupata suluhisho la tatizo la goti ambalo limekuwa likimsumbua kwa muda mrefu.
Uhuru alisema anaamini mazungumzo ya ana kwa ana na Makonda yatampa fursa ya kueleza changamoto yake, huku akisisitiza kuwa lengo lake ni kutafuta msaada alioukosa kwa muda mrefu tangu akiwa mchezaji wa mpira katika timu ya Simba.
“Natamani kukutana na Makonda. Najua amewasaidia watu wengi na naamini hata mimi atanisaidia kutatua tatizo langu la muda mrefu,” alisema Uhuru.
Uhuru, ambaye aliitumikia Simba kwa mafanikio makubwa enzi za uchezaji wake, amesema maumivu ya goti yameendelea kumsumbua kwa muda mrefu licha ya kuendelea na majukumu yake kama kocha wa viungo wa KMC.
Amesema ana matumaini kuwa akipata nafasi ya kuonana na Makonda, huenda akapata msaada utakaomuwezesha kupata suluhisho la changamoto hiyo iliyodumu kwa miaka mingi.




