Ligi Kuu

Kiemba, Domayo watua Kagera Sugar

KAGERA: KAGERA Sugar imeendelea kuimarisha benchi lake la ufundi baada ya kuwatambulisha Amri Kiemba na Frank Domayo kuwa makocha wasaidizi chini ys Kocha Mkuu, Cedric Kaze, huku Kefa Mabala akiteuliwa kuwa mchambuzi wa video.

Katika taarifa ya klabu hiyo iliyotolewa leo Kiemba ametambulishwa kuwa Kocha Msaidizi namba moja, wakati Domayo ameingia kwenye benchi hilo kama Kocha Msaidizi namba mbili, katika maboresho yanayolenga kuongeza nguvu katika maandalizi ya kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu.

Kiemba, ambaye aliwahi kuzitumikia Simba, Yanga, Azam na Kagera Sugar pamoja na Taifa Stars akiwa mchezaji, pia ana uzoefu wa uchambuzi wa soka na amewahi kuwa sehemu ya benchi la Taifa Stars kama kocha msaidizi.

Kwa upande wake, Domayo ni kiungo wa zamani aliyewahi kucheza katika klabu kubwa za Yanga na Azam pamoja na Taifa Stars na, kama Kiemba, amekuwa akijikita pia katika uchambuzi wa soka huku akiendelea na safari ya kupata uzoefu katika taaluma ya ukocha.

Mabala naye ameingizwa kwenye benchi hilo kama mchambuzi wa video, nafasi inayotarajiwa kusaidia benchi la ufundi katika kuchambua mwenendo wa timu, wapinzani na maeneo yanayohitaji maboresho.

Ujio wa watatu hao ni sehemu ya hatua za Kagera Sugar kuimarisha benchi la Kaze, ambaye aliteuliwa baada ya klabu hiyo kuachana na Juma Kaseja kufuatia matokeo yasiyoridhisha katika mwanzo wa msimu.

Kagera ilikuwa imekusanya pointi mbili katika mechi sita za kwanza, ikipata sare mbili na kupoteza nne.

Kagera Sugar inatarajiwa kutumia mapumziko ya ligi kufanya maboresho zaidi kuelekea michezo ijayo.

Related Articles

Back to top button