Ligi Kuu

Simba, Pamba Jiji kibaruani Kirumba

MWANZA: SIMBA SC leo itakuwa na kibarua kingine katika harakati zake za kuendelea kujiimarisha katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara, itakapokuwa mgeni wa Pamba Jiji kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na morali baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo uliopita, wakati Pamba Jiji yenyewe ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Dodoma Jiji.

Pamoja na tofauti ya viwango na malengo ya timu hizo, Simba haitakuwa na safari rahisi Mwanza, kwani Pamba itakuwa mbele ya mashabiki wake ikiwa na kiu ya kupata matokeo mazuri dhidi ya moja ya timu kubwa nchini.

Msimu uliopita, Pamba Jiji ilifanikiwa kuizuia Simba nyumbani baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1, matokeo yanayoweza kuongeza hamasa kwa wenyeji kuelekea mchezo wa leo.

Simba inaweza kuwa na kikosi chenye uzoefu na ubora mkubwa, lakini Pamba imeonesha kuwa inaweza kuwa na ushindani inapokutana na timu zenye majina makubwa. Hivyo, dakika 90 za mchezo ndizo zitakazotoa jibu la nani atatawala Kirumba.

Kwa Simba, ushindi utakuwa muhimu katika kuendeleza mwendo mzuri wa ligi na kuongeza kujiamini, wakati Pamba ikisaka pointi muhimu mbele ya mashabiki wake ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo.

Michezo mingine itakayochezwa leo ni Kagera Sugar dhidi ya Singida Black Stars huku Mbeya City ikitarajiwa kuwakaribisha Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.

Related Articles

Back to top button