Italian Super Cup kuwashwa India?

BANGALORE, Mkurugenzi wa masoko na promosheni wa Ligi kuu ya Italy maarufu kama Serie A Michele Ciccarese amesema uongozi wa Ligi hiyo unafikiria kupeleka michezo wa Italian super cup nchini India katika kile alichotaja kuwa ni kutanua mashindano hayo na kuongeza mashabiki.
Alipoulizwa kuhusu tetesi za shindano hilo kupelekwa nchini India Ciccarese alithibitisha na kusema kuwa kupeleka mashindano hayo India kunaenda sambamba na mpango mkakati wa ligi hiyo wa kutanua mbawa zake ulimwenguni.
“Tunachotaka kufanya ni kuyasambaza mashindano yetu kama Super Cup kote ulimwengu kwa sababu moja tu, kupata mashabiki na kupeleka utamaduni wa soka letu duniani. Kwa hiyo ni jambo ambalo tunaweza kufanya, mazungumzo tu na tutakuja kucheza hapa” amesema Ciccarese
Makala iliyopita ya Italian Super Cup ilipigwa nchini Saudi Arabia ikishirikisha bingwa wa Ligi kuu Serie A na mshindi wa pili pamoja na bingwa na mshindi wa pili wa Coppa Italia ikishuhudiwa AC Milan ikiifunza adabu Inter Milan kwa mabao 3-2 na kutwaa kombe hilo kwa mara ya 8.
Ciccarese yupo nchini India kuhudhuria kilele cha mkutano wa ubunifu wa michezo nchini India unaofanyika katika jiji la Bangalore.