Mzee Yusuph Mwinyi:Amani ianze ngazi ya familia

DAR ES SALAAM:MZEE Yusuph Mwinyi amesema kuwa matumizi ya maneno mabaya dhidi ya wengine ni uvunjifu wa amani unaoweza kusababisha hofu na wasiwasi katika jamii.
Akizungumza na SpotiLeo, Mzee Yusuph amesema kuwa amani inapaswa kuanzia ndani ya familia kabla ya kuenea katika jamii na taifa kwa ujumla.
Ameeleza kuwa hata kumfokea mke au mwanafamilia bila sababu ni kitendo kinachochangia kuvuruga amani.
“Tunapaswa kujenga na kudumisha amani kuanzia ngazi ya familia hadi taifa. Hali hiyo itasaidia amani kukua na kuenea zaidi nchini,” amesema.
Aidha, Mzee Yusuph amewataka wasanii kutumia vipaji vyao kuhamasisha amani kupitia nyimbo zao, akisisitiza kuwa sanaa ni chombo muhimu cha kuelimisha na kuunganisha jamii.
Ameongeza kuwa ushirikiano wa wananchi na wadau mbalimbali katika kuhubiri amani utachangia kudumisha utulivu na maendeleo ya taifa.




