Guirassy: Ilikuwa ngumu kuziba gepu lile

DORTMUND:MSHAMBULIAJI wa Borussia Dortmund Serhou Guirassy amesema klabu yake imeondoshwa kwenye michuano ya Ligi ya mabingwa barani Ulaya kutokana na idadi kubwa ya mabao walioruhusu kwenye mzunguko wa kwanza hivyo kuweka ugumu wa kuziba gepu la mabao 4-0 la mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Barcelona.
Guirassy aliyeanza kufufua matumaini ya Dortmund kwa penati ya dakika ya 11 amesema anaamini iwapo wangecheza vizuri mzunguko wa kwanza na kutoruhusu kufungwa au kufungwa mabao machache wangeweza kuiondoa FC Barcelona kwenye michuano hiyo.
“Kama wao Sisi pia ni timu bora na tumeonesha hilo leo, bahati mbaya tu gepu lilikuwa kubwa sana, ni ngumu kuziba tulifanya vibaya mchezo wa kwanza pengine tusingefungwa idadi ile ya mabao tungekuwa na hadithi tofauti sasa hivi” Guirassy ameiambia Amazon prime.
Mshambuliaji huyo ambaye alifunga hat-trick katika mchezo huo wa jana usiku dhidi ya Barcelona na kuwa kinara wa mabao msimu huu akiwa na mabao 13 akiwapita Raphinha na Lewandowski wa Barcelona amesema pia anajisikia furaha kiasi kuwa kinara wa mabao lakini ana huzuni kubwa ya kushindwa kufika walipoishia msimu uliopita.
Borussia Dortmund walicheza fainali ya UEFA Champions League dhidi ya Real Madrid msimu uliopita na kupoteza mbele ya vigogo hao wenye ‘kismati’ na ligi hiyo. Msimu huu wameondolewa na timu nyingine ya Spain katika hatua ya robo fainali kwa Aggregate ya 5-3.