Yanga na matumaini makubwa Lubumbashi

DAR ES SALAAM: KIKOSI cha Yanga kimeondoka leo nchini kuelekea Lubumbashi na matumaini ya kusaka pointi muhimu katika mchezo wa tatu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.
Mkurugenzi wa ufundi wa Yanga, Abdihamid Moalin amesema wamefanya kazi kubwa ya kuboresha madhaifu yaliyojitokeza katika mchezo uliopita na kuwataka wachezaji kusahau matokeo ya mchezo huo na sasa akili na nguvu dhidi ni ya TP Mazembe.
“Tumefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza mechi iliyopita,tumepoteza michezo miwili lakini bado hatujaondoka katika malengo yetu, tumejipanga vizuri na tupo tayari kusaka alama muhimu dhidi ya TP Mazembe,” amesema.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema kikosi kimeondoka asubuhi, na mchana wa leo watawasili Lubumbashi na kufanya mazoezi kulingana na programu ya kocha Saed Ramovic kwa ajili ya mchezo huo.
“Wachezaji wote wapo imara akiwemo Chadrack Boka ambaye hakuwepo kwenye mchezo uliopita kutokana na majeraha, ila suala la kucheza litakuwa ni mipango ya kocha lakini tutakosa huduma ya Aziz Andambwile ambaye bado hayuko vizuri anafanya mazoezi mepesi,” amesema.
Kamwe amesema hawajakata tamaa na hawatayumbishwa kabisa na matokeo ya michezo miwili iliyotangulia na wanaamini nafasi ya kupambania pointi 12, imani yao ipo katika kundi la wachezaji kupata matokeo Lubumbashi.