Africa

Gamondi amrejesha Manula Taifa Stars

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Taifa Stars Miguel Gamondi amemrejesha kikosini kipa wa Azam Aishi Manula kwenye kikosi cha wachezaji 25 kitakachoingia kambini kujiandaa na michezo ya Fifa Series 2026.

Manula aliwahi kutumikia Taifa Stars akiwa Simba baadaye akapata majeraha yaliyomweka nje kwa muda mrefu n a hata alivyopona hakupata nafasi hadi alipojiunga na Azam FC ambapo amekuwa na kiwango bora hivi karibuni.

Katika kikosi hicho, wapo wachezaji walioonekana kwenye fainali za Afrika za Morocco 2025 hawajaitwa wakiwemo Shomari Kapombe, Dikson Job ambaye ni majeruhi, Mbwana Samatta, Pascal Msindo,Kibu Denis, Hussein Masalanga na Lusajo Mwaikenda. Kuna sura mpya kadhaa zikiwemo kipa wa Pamba Yona Amis, Paul Peter wa JKT Tanzania, Twalibu Nuru wa Azam  na Mohamed Mussa wa Mashujaa.

Wengine walioitwa ni pamoja na Zuberi Foba, Elias Lameck na Feisal Salum (Azam FC), Bakari Msimu (Coastal Union), Haji Mnoga (Salford City, England), Nickson Kibabage, Yusuph Kagoma na Suleiman Mwalimu (Simba SC).

Pia wamo Bakari Mwamnyeto, Mohamed Hussein, Mudathir Yahya na Ibrahim Bacca (Yanga SC), Kelvin Nashon (Pamba), Novatus Dismas (Göztepe, Uturuki), Alphonce Mabula (Shamakhi, Azerbaijan), Simon Msuva (Al Talaba, Iraq), Kelvin John (Aalborg, Denmark), Charles Mmombwa (Floriana FC, Malta) na Tarryn Allarakhia (Rochdale, England).

Taifa Stars itaanza kampeni yake kwa kucheza dhidi ya Liechtenstein Alhamisi ya Machi 26, 2026, kabla ya kushuka tena dimbani Jumapili ya Machi 29, 2026 dhidi ya mshindi au mshindwa wa mchezo kati ya Aruba na Macau.

Katika michuano hiyo, timu zimegawanywa katika makundi mawili ambapo kundi A linaundwa na Rwanda, Kenya, Estonia na Grenada.

Kundi B ambalo ipo Tanzania linajumuisha Liechtenstein, Aruba na Macau.

Michuano yote ya makundi A na B inatarajiwa kuchezwa nchini Rwanda.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button