Furahisha atoa vitisho kwa mpinzani
BONDIA Hamad Furahisha amemtahadharisha mpinzani wake Ally Mazome kuwa ajiandae kisaikolojia kwani kipigo alichomwandalia hatokisahau katika maisha yake.
Furahisha atapambana na bondia wa Morogoro Ally Mazome katika pambano lililopewa jina la homa ya SGR litakalofanyika Oktoba 25, mwaka huu mkoani Morogoro.
Akizungumzia maandalizi yake Furahisha amesema hawataenda mkoani humo kutalii bali kuonesha uwezo wa kurusha ngumi na kumfundisha kazi Mazome.
“Wenyewe wanaelewa walipita mabondia wengi hapa, kwa hiyo wakae mkao wa kula, nitume tu salama kwako Ally tunakuja imara tarehe 25 kuuwasha moto na kuondoka na ushindi,”amesema.
Kocha wake Furahisha, Haji Pera amesema hawana kazi mbovu kwa namna alivyomwandaa bondia wake ana imani atafanya vizuri.
“Kichaka cha Chui huwa haingii Simba, mpinzani wa Furahisha cha moto atakiona, kazi zetu zinaeleweka. Tuwe na mechi au tusiwe nayo lazima mazoezi ya nguvu yafanyike ndicho ambacho kimekuwa kikifanyika kumuandaa mchezaji wangu muda wowote na tayari kwa mazoezi,”amesema.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Yombo Dovya Rashid Mbanga anakoishi bondia huyo amesema kwa namna anavyomwamini kijana wake kwa uwezo wapinzani wajiandae vizuri vinginevyo kazi wanayo.