Masumbwi

Vunjabei, Macho waitwa timu ya taifa ya ngumi

DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Ngumi Tanzania (BFT) limetangaza mabondia 15 wa timu ya taifa ya ngumi watakaoingia kambini kujiandaa na mashindano ya ubingwa wa dunia kwa wanawake.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa BFT Makore Mashaga kwa vyombo vya habari, uteuzi huo umekuja baada ya kumalizika kwa mashindano ya Samia Women Boxing Championship yaliyofanyika Dar es Salaam wiki iliyopita.

Mashindano hayo ya dunia yanatarajiwa kufanyika kuanzia Machi 6 hadi 17 mwaka huu nchini Serbia.

Majina ya mabondia waliochaguliwa kuunda kikosi cha timu ya taifa ni pamoja na Halima Vunjabei uzito wa kilo 57 kutoka kundi la Nakoz, Zulfa Macho kutoka Ngome uzito wa kilo 52.

Halima Vunjabei ndiye bingwa wa mkanda wa ubingwa wa mabara wa WBF baada ya kumchakaza mpinzani wake Songuel Ayten raia wa Uturuki raundi ya tatu nchini Ujerumani Novemba mwaka jana.

Wengine walioitwa ni Veronika Thomas (MMJKT) Uzito wa kilo 48, Latifa Said (JKT) uzito wa kilo 50 sawa na Sarafina Fusi (NGOME), Tatiana Ezekiel (ZUGO) uzito wa kilo 54, Vumilia kalinga (NGOME) uzito wa kilo 57 sawa na Zawadi Amosi.

Wengine ni Doricas Daudi (KWAME) na Zulfa Iddi (ZOGO) uzito wa kilo 60, Najma Isike (TAIFA) uzito wa kilo 63, Konsolata Laiza (POLISI ARUSHA) uzito wa kilo 66, Salma Michael (MWANZA) uzito wa kilo 75 na Rachel Msingo (DODOMA) na Mariam Msabila (KINYOGOLI) uzito wa kilo 81.

Mashaga amesema timu hiyo itaanza mazoezi rasmi Jumatatu ya Februari 10, mwaka huu kwa mtindo wa kuja mazoezini na kurudi majumbani, wakati BFT likiwa katika mipango ya kutafuta pesa za kuweza kuwaweka katika kambi ya pamoja na pesa za safari ya kwenda Serbia kushiriki mashindano hayo.

“Timu hiyo itaendelea kufundishwa na Kocha Mkuu Samwel Kapungu akisaidiana na Mzonge Hassani na Muhsini Mohamed hadi hapo yatapofanyika maamuzi mengine, mabondia 12 ndio watakaosafiri kuelekea Serbia,”ilisema taarifa ya Mashaga.
Mwisho

Related Articles

Back to top button