Federal Da General awapa tano marapa Afrika

RAPA mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambaye kwa sasa anaishi Marekani, Federal Da General, amewaomba wapenzi wa muziki wa rap Afrika Mashariki kuipokea projekti yake mpya Dropicana Assa Anna.
Federal amewaahidi sifa marapa nyota kutoka Afrika Mashariki, akiwataja kama kielelezo cha mapinduzi ya muziki wa rap ndani na nje ya bara la Afrika, jambo linalowavutia mashabiki wengi.
Akizungumza na Spotileo, Federal Da General alisema licha ya kuishi Marekani kwa muda mrefu, ameendelea kuwasikiliza marapa kutoka Afrika Mashariki kwa sababu anajifunza kutoka kwao.
“Bado najifunza mengi kutoka kwa kaka zangu huko Afrika na huku Marekani. Ukisikiliza wimbo wangu mpya Dropicana Assa Anna ambao video yake inapatikana kwenye chaneli yangu ya Vevo, utaelewa ninachomaanisha. Naendelea kujenga jina na heshima yangu Afrika Mashariki kupitia muziki huu wa rap, ambao umekuwa chanzo cha ustawi kwa wasanii wengi matajiri Marekani,” alisema Federal.
Alimalizia kwa kuwaomba mashabiki wa rap kumsapoti na kufuatilia kazi zake kwenye mitandao yake ya kijamii kama vile Instagram, Facebook, TikTok, Twitter, Spotify, na YouTube kwa jina la Federal Da General. Alisisitiza kuwa akifanikiwa, atakuwa daraja la kuwasaidia vijana wengine Afrika.