Fayvanny na warembo kunogesha Tanzania Fashion Festival 2026

DAR ES SALAAM: JUKWAA la ubunifu wa mavazi nchini, Tanzania Fashion Festival, msimu wa saba linatarajiwa kunogeshwa na mbunifu na Video Queen, Fayvanny, litakalofanyika Septemba 26, mwaka huu katika ukumbi wa Terrace Slipway, Masaki jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Spoti Leo, Msemaji wa Tz fashion festival, Bhoke Egina’, amesema kila msimu umekuwa na utofauti wake, huku mwaka huu wakitarajia kumpokea Fayvanny kama mgeni rasmi.

Amesema pia jukwaa hilo litawakutanisha warembo mbalimbali, akiwemo Miss Grand Tanzania, Beatrice Alex na Miss Grand Kilimanjaro, Tess Kessy, ambao watashiriki katika kulifanya jukwaa hilo kuwa la kipekee.
“Kila msimu tunakuwa na utofauti. Mwaka huu tumepata muitikio mkubwa kutoka kwa warembo, hivyo tumeamua kuwapa nafasi zaidi kushiriki katika jukwaa hili,” amesema Deo.
Amesema Tanzania Fashion Festival inalenga kukuza sanaa za maonyesho, kuibua vipaji vipya na kuwapa nafasi wabunifu wachanga kuonyesha kazi zao bila gharama.
“Lengo la jukwaa hili ni kuendeleza na kukuza sanaa za maonyesho, kuibua na kuunga mkono vipaji vipya vinavyochipukia. Mbunifu anatakiwa kuandaa mavazi yake na kuja kuyaonyesha katika jukwaa hili bila gharama,” amesema.

Deo amesema tamasha hilo litawakutanisha mastaa mbalimbali kutoka katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva, filamu, mitindo na sanaa nyingine za maonyesho, pamoja na viongozi na wadau wa tasnia.
Amesema aliamua kuanzisha jukwaa hilo kutokana na kutambua mchango wake katika tasnia ya ubunifu wa mavazi na kutaka kuwainua wabunifu wachanga.
“Kwa kutambua mchango wangu katika tasnia ya ubunifu wa mavazi nchini, niliamua kuandaa jukwaa hili ili kuibua wabunifu wachanga na kuzidi kuipa nafasi tasnia ya mavazi nchini,” amesema.
Aidha, amesema Tanzania Fashion Festival imekuwa ikifungua fursa kwa wanamitindo na wabunifu wa ndani na nje ya nchi kujitangaza na kupata nafasi ya kutambulika zaidi kutokana na wageni mbalimbali wanaohudhuria na kuvutiwa na kazi zinazowasilishwa jukwaani.
Amesema msimu huu umeandaliwa kwa namna ya kipekee zaidi ili kuongeza burudani na fursa za kibiashara kwa washiriki na wadau wa tasnia.
Hata hivyo, amewataka wadau na wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kudhamini jukwaa hilo ili liendelee kuwa sehemu muhimu ya kukuza vipaji na biashara katika sekta ya mitindo nchini.




