Fadlu: Wakijaa kipindi cha kwanza tu mechi imeisha
DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema ana kazi ya kufanya kwenye safu ya ushambuliaji ili kuwa tishio na kumaliza mechi katika kipindi cha kwanza kwa kupata idadi kubwa ya mabao.
Amesema wanapotumia vizuri nafasi wanazotengeneza kwa kufunga mabao mengi kipindi cha kwanza itawasaidia kucheza bila shinikizo kipindi cha pili kwa kudhibiti na kumiliki mchezo.
Fadlu amesema mechi iliyopita dhidi ya Tabora United walipata nafasi nyingi kipindi cha kwanza lakini wakashindwa kuzitumia na hivyo anafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza na ndio maana wameongeza mshambuliaji mwingine ndani ya kikosi hicho.
Amesema kikosi kinaelekea kwenye ubora anaohitaji, na ana uhakika wa kuwa na timu tishio kwa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara na Afrika kwa kuwa wanaanza kuimarika siku hadi siku.
“Bado nina kazi ya kufanya, baada ya mechi iliyopita dhidi ya Tabora United ilikuwa tumalize mchezo kipindi cha kwanza, cha pili tucheze bila presha kwa kuzuia na kuumiliki mchezo, haikuwa hivyo”amesema Kocha huyo.