Filamu ya Mvera kuipeleka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa

DAR ES SALAAM: Bodi ya Filamu Tanzania imeshiriki katika onyesho maalumu la filamu ya Mvera lililofanyika katika Kituo cha Sayansi na Utamaduni cha Urusi (Russian House), jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza tasnia ya filamu na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.
Filamu ya Mvera ni miongoni mwa filamu sita zilizoteuliwa na mtandao wa Film Africa Network (FAN) kuoneshwa katika nchi 21 barani Afrika, hatua inayotoa fursa kwa kazi za filamu za Kiafrika kuwafikia watazamaji wengi zaidi ndani na nje ya mipaka ya nchi zao.
Kupitia programu hiyo, Tanzania imepata nafasi ya kuwa miongoni mwa vituo vya maonesho hayo, ambapo Mvera imekuwa filamu ya pili kuoneshwa nchini kupitia ukumbi wa Russian House, baada ya Nigeria kuwa nchi ya kwanza kufungua rasmi mfululizo wa maonesho hayo.
Onesho hilo lilifunguliwa rasmi na Mkurugenzi wa Kituo cha Sayansi na Utamaduni cha Urusi nchini Tanzania, Alexander Evstigneev, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa tasnia ya filamu, akiwemo Profesa Martin Mhando.
Uratibu wa onesho hilo ulifanywa na Goima Mwamwingila, ambaye ni mwakilishi wa Film Africa Network nchini Tanzania.
Ushiriki wa Bodi ya Filamu Tanzania katika tukio hilo unaonesha dhamira ya kuendelea kuunga mkono majukwaa yanayotoa fursa kwa watengenezaji wa filamu kuonesha kazi zao, kubadilishana uzoefu na kujenga mitandao ya ushirikiano wa kimataifa.
Aidha, ushirikiano kati ya Bodi ya Filamu Tanzania, Film Africa Network na Kituo cha Sayansi na Utamaduni cha Urusi unatajwa kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kukuza filamu za Kitanzania na kuimarisha nafasi ya nchi katika tasnia ya filamu barani Afrika.




