Kwingineko

Clara Luvanga akumbuka nyumbani Tanzania

DAR ES SALAAM: MSHAAMBULIAJI wa Tanzania, Clara Luvanga, amesema mambo anayoyakosa zaidi akiwa Marekani ni kuwa karibu na familia yake pamoja na vyakula vya Kitanzania.

Clara, anayeitumikia klabu ya Washington Spirit inayoshiriki Ligi ya Wanawake ya Marekani (NWSL), ameeleza hayo baada ya kuulizwa na klabu yake mambo anayoyakumbuka zaidi kutoka Tanzania.

Nyota huyo amesema licha ya kufurahia changamoto mpya ya soka nchini Marekani, bado anakumbuka ukaribu wa familia yake na vyakula vya nyumbani, vitu anavyovikosa akiwa mbali na Tanzania.

Hata hivyo, maisha yake mapya Marekani yameanza kuzaa matunda, baada ya kuanza kuonesha uwezo wake katika kikosi cha Washington Spirit tangu alipojiunga nacho Septemba mwaka huu.

Clara tayari amefunga mabao mawili na kutoa asisti moja, akionesha mchango wake katika safu ya ushambuliaji licha ya kuwasili wakati msimu ukiwa umeendelea.

Bao lake la kwanza katika ligi hiyo alifunga dhidi ya Houston Dash Oktoba 4, kabla ya kuongeza jingine dhidi ya Kansas City Current Oktoba 25, huku pia akitoa pasi ya bao katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Chicago Stars Novemba 1.

Usajili wake kwenda Washington Spirit ulimfanya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi ya Wanawake ya Marekani, baada ya kusaini mkataba wa miaka minne utakaomuweka klabuni hapo hadi 2029.

Kabla ya kuhamia Marekani, Clara aliitumikia Al Nassr ya Saudi Arabia kwa mafanikio makubwa, akishinda mataji matatu ya ligi na kutwaa kiatu cha dhahabu msimu uliopita baada ya kufunga mabao 24.

Related Articles

Back to top button