Dar City yatinga nusu fainali kufuzu Ligi Afrika

NAIROBI: TIMU ya mpira wa kikapu ya Dar City imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya kufuzu Ligi ya Afrika 2027, baada ya kuichapa Namuwongo Blazers ya Uganda kwa vikapu 91-79.
Ushindi huo uliopatikana katika mchezo wa makundi uliochezwa jijini Nairobi, Kenya, umeiweka Dar City katika nafasi nzuri ya kuendelea na safari ya kusaka tiketi ya kushiriki mashindano ya BAL 2027.
Mchezo huo umekuwa wa pili kwa Dar City katika hatua ya makundi, baada ya kuanza kampeni yake kwa ushindi wa vikapu 96-76 dhidi ya Ferroviario da Beira ya Msumbiji, matokeo yaliyoonesha uimara wa kikosi hicho kinachonolewa na kocha Mamadou Gueye.
Dar City sasa itakuwa na mchezo mmoja wa kukamilisha ratiba ya kundi B dhidi ya Dolphins Basketball ya Botswana, utakaochezwa Novemba 26, ambapo ushindi au matokeo mazuri yataisaidia timu hiyo kujiweka katika nafasi nzuri kuelekea hatua inayofuata.
Kwa mujibu wa mfumo wa mashindano hayo, timu mbili za juu kutoka kila kundi zitatinga nusu fainali itakayochezwa Novemba 28, huku fainali na mchezo wa kuwania nafasi ya tatu vikipangwa kufanyika Novemba 29 jijini Nairobi. FIBA




