Feisal: Utu na upendo ni muhimu kuliko kulinda brand

DAR ES SALAAM: MCHEZAJI wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, amesema utu, upendo na kudumisha urafiki wa muda mrefu ni mambo yenye thamani kubwa kuliko kujali taswira ya umaarufu wake (brand), akisisitiza kuwa maisha ya binadamu ni mafupi.
Feisal amesema amekuwa na marafiki tangu akiwa mtoto na amedumisha ukaribu nao hadi sasa, kiasi kwamba kila anaporejea nyumbani, utaratibu wake ni kuhakikisha anakutana nao na kufurahia muda pamoja.
Akizungumzia suala la kulinda brand, mchezaji huyo amehoji umuhimu wa watu kujikita zaidi katika kuhifadhi taswira ya umaarufu huku wakisahau misingi ya utu na mahusiano mema na jamii inayowazunguka.
“Kurinda brand ndiyo nini? Brand inaisha, shehe. Kuna wachezaji wengine wanalinda brand zao lakini mwisho wa siku wanasahaulika. Hapa duniani leo tupo, kesho tunaondoka,” amesema Feisal.
Ameongeza kuwa jambo la msingi katika maisha si kujenga jina pekee, bali ni namna mtu anavyowatendea wengine na nafasi anayowapa watu katika maisha yake.
Kwa mujibu wa Feisal, upendo unapopewa nafasi katika mahusiano, hujenga heshima na kufanya watu wakuthamini bila kujali kiwango cha umaarufu au mafanikio uliyonayo.
Kauli hiyo inaweka msisitizo katika umuhimu wa wachezaji na watu maarufu kuendelea kuwa na uhusiano mzuri na jamii zao, bila kuruhusu umaarufu kuwabadilisha na kuwasahaulisha watu waliokuwa sehemu ya safari yao ya maisha.




