COSOTA kugawa Sh bilioni 1.3 kwa wabunifu

DAR ES SALAAM: OFISI ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) inatarajia kugawa Sh bilioni 1.3 kwa wasanii na wabunifu nchini Novemba 26 mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wa tozo ya hakimiliki ulioanzishwa kwa lengo la kuhakikisha wabunifu wananufaika na kazi zao.
Mgawo huo utafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, ikiwa ni utekelezaji wa tangazo lililotolewa awali na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, katika mkutano wake na waandishi wa habari Septemba mwaka huu.
Akizuzungumza na waandishi wa Habari Dar es Salaam leo Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki wa COSOTA, Naomi Mungure, amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh bilioni 2.3 kuanzia Septemba 2023 hadi Juni 2026 kupitia tozo hiyo, ambapo asilimia 60 ya fedha hizo, sawa na Sh 1.3 ndizo zitakazogawiwa kwa walengwa.
“Tozo hiyo ilianzishwa kufuatia maboresho ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2022, baada ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kulinda maslahi ya wabunifu na kuwawezesha kupata manufaa ya kiuchumi kutokana na kazi zao,”amesema.
Mungure amesema tozo hiyo ya asilimia 1.5 inatozwa kwa vifaa vinavyotumika kuzalisha, kunakili, kusambaza na kuhifadhi kazi za sanaa na uandishi, vinapoingizwa kutoka nje ya nchi au vinapozalishwa na kuundwa nchini, huku ukusanyaji wake ukisimamiwa na TRA.
Amesema jumla ya aina 13 za vifaa zimeainishwa kutozwa, zikiwamo CD, DVD, Digital Jukebox, MP3 Player, SD Memory Card, Vinyl, Mini Disc, Compact Disc, redio na televisheni zenye uwezo wa kurekodi, pamoja na vifaa vya kurekodi sauti na picha.
Walengwa wa mgawo huo wamegawanywa katika makundi matano ambayo ni wabunifu wa muziki, filamu, maandishi, sanaa za ufundi na sanaa za maonesho, kwa kuzingatia mwongozo wa sheria na kanuni zinazosimamia tozo hiyo.
Hatua hiyo pia inaendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayosisitiza uchumi na ubunifu, pamoja na kuhakikisha wabunifu wanapata haki na manufaa yanayotokana na kazi zao.
Akizungumzia utekelezaji wa mfumo huo, Mungure amesema utaratibu wa kukusanya tozo ya hakimiliki unatumika pia katika mataifa mengine yakiwamo Kenya, Malawi, Algeria, Ghana, Tunisia, Burkina Faso na Morocco, huku Canada, Marekani, Ufaransa, Australia, Ujerumani na Ubelgiji yakiwa miongoni mwa nchi zinazotekeleza mfumo huo.
Ameishukuru Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kusimamia mchakato wa ukusanyaji na ugawaji wa fedha hizo, akisema tozo hiyo imeongeza wigo wa mapato kwa wasanii na waandishi na kuimarisha mazingira ya wabunifu kunufaika na kazi zao.




