Kwingineko

Clarke kuendelea kuinoa Scotland hadi 2030

EDINBURG: KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Scotland, Steve Clarke, ameongeza mkataba mpya utakaomuweka madarakani hadi Kombe la Dunia la mwaka 2030 baada ya mafanikio ya kuifikisha nchi hiyo katika fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza baada ya miaka 28.
Clarke mwenye umri wa miaka 62 alikuwa katika sintofahamu kuhusu hatma yake licha ya kuiwezesha Scotland kufuzu michuano miwili mfululizo ya Euro pamoja na Kombe la Dunia la 2026 litakalofanyika Marekani.
Kocha huyo aliyeteuliwa mwaka 2019 amesema ana heshima kubwa kuendelea kuiongoza Scotland katika kipindi hicho muhimu cha mpira wa miguu nchini humo.
“Nina heshima kubwa kuiongoza Scotland katika Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza baada ya miaka 28 na ninafurahia kuendelea kuwa kocha mkuu wa timu hii,” amesema Clarke.
Amesema mafanikio ya kufuzu michuano mikubwa yameonyesha maendeleo makubwa ya kikosi hicho huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kujenga msingi imara wa timu kwa miaka ijayo.
Katika kipindi chake cha uongozi, Clarke ameiongoza Scotland kucheza mechi 76 akishinda 33, sare 16 na kupoteza 27, huku akiweka rekodi ya kuwa kocha aliyefanikiwa zaidi katika historia ya timu hiyo kwa kufuzu mashindano makubwa matatu.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Scotland, Ian Maxwell, amesema Clarke ameonesha dira mpya na nia ya kuendelea kuiboresha timu hiyo kwa muda mrefu.
Hata hivyo, uamuzi wa kuongeza mkataba wake umezua mjadala mkubwa kwa mashabiki wa Scotland, ambapo baadhi wamepongeza mwendelezo wake huku wengine wakihofia timu hiyo inaweza kuendelea kufanya vibaya katika mashindano makubwa.
Scotland inatarajia kuanza kampeni yake ya Kombe la Dunia 2026 kwa mchezo dhidi ya Haiti mjini Boston mwezi ujao.

Related Articles

Back to top button