Chama, Yanga ndoto za Abunuasi
DAR ES SALAAM. KITENDAWILI cha Hatma wa kiungo wa Simba, Clatous Chama kimetagulia baada ya nyota huyo kuongeza mkataba wa miaka miwili kusalia ndani ya kikosi cha wekundu hao wa Msimbazi kwa msimu ujao wa Mashindano.
Chama mkataba wake umefikia ukingoni na ilidaiwa kuwa nyota huyo amekuwa na mazungumzo na Rais wa klabu ya Yanga, Hersi Said kwa ajili ya kusajiliwa na Mabingwa wa Ligi Kuu Bara mara 30, Yanga.
Taarifa zilizopatikana ni kuwa Chama amekuwa akihusishwa na Yanga kila msimu, ameshamalizana na Waajiriwa wake Simba kwa kuongeza mkataba wa miaka miwili mingine kutumikia klabu hiyo katika mashindano kwa msimu ujao.
Spotileo leo ilimtafuta Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally ambaye amesema watamwongezea mkataba mchezaji yeyote ambaye amemaliza mkataba na bado anahitajika kuendelea kusalia ndani ya kikosi cha Simba.
Ahmed amesema Simba haishindwi kumuongezea mkataba mchezaji yeyote wenye malengo naye kwa sababu ya kifedha labda mchezaji atakae kuondoka mwenyewe na ataondoka.
“Mchezaji yoyote Simba tunahitaji kubaki naye msimu ujao basi tutatoa gharama yoyote tutambakiza isipokuwa yule ambaye atakuwa amepata ofa nyingine na sio ndani hapa.
Mwekezaji na Rais wa Heshima, Mohamed Dewji ameweka mzigo mezani, hakuna mchezaji anayetakiwa na Simba akaondoka kisa fedha. Huyo Chama wamekuwa wakimsajili kila msimu na anabaki katika viunga vya Msimbazi,” amesema Ofisa habari huyo.
Ameongeza kuwa usajili wa safari hii upo kwenye mikono salama ukisimamiwa kwa umakini Mo Dewji kuhakikisha wanafanya usajili mzuri kwa kuboresha kikosi kwa ajili ya msimu ujao wa kombe la Shirikisho la Afrika.
Ahmed amewataka mashabiki kuwa watulivu, wanatambua msimu huu hawakufanya vizuri na kusahihisha makosa ya ikiwemo kufanya usajili wa wachezaji bora watakaowapa matokeo.
Simba hawakufanya vizuri msimu huu kwenye ligi na kumaliza nafasi ya tatu katika msimamo na kupoteza nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao .
Pia wameondolewa katika hatua ya robo fainali ya kombe la Shirikisho la CRDB Bank dhidi ya Mashujaa FC, mchezo uliopigwa Uwanja wa Lake Tanganyika. Kigoma.