CEO mpya wa Simba, moto wa kuotea mbali
DAR ES SALAAM: MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugezi wa Simba, Mohammed Dewji amemtangaza rasmi mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Uweyezu Francois Regis kuchukuwa nafasi ya Imani Kajula anayemaliza muda wake Julai 31, 2024.
Taarifa iliyotolewa na Dewji, imesema Ofisa Mtendaji huyo mpya wa Simba, ni mwenye ujuzi na uzoefu katika utawala wa soka na fedha bila shaka ataifanya klabu hiyo kufikia viwango vipya ili kuhakikisha ukuaji thabiti wa shirika na utendaji ulioimarishwa ndani na nje ya uwanja.
“Napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Iman Kajula, kwa niaba yangu na bodi kwa mchango mkubwa alioufanya Simba unaacha alama chanya za maendeleo na mafanikio,ayatakuwa ya juu zaidi kutoka pale Simba itaendelea kukua,” amesema Mo Dewji.
Amesema wamemteuwa mtendaji mpya baada ya Kajula kujiuzulu miezi michache iliyopita na kufikia Agosti 31, anamkabidhi majukumu Regis kuwa ofisa Mtendaji wetu mpya kuanzia tarehe 1 Agosti 2024
Regis aliyewahi kuwa kiongozi wa Shirikisho la mpira wa Miguu nchni Rwanda, mtaalamu na mbunifu na mwenye zaidi ya miaka kumi na mbili ya uzoefu katika soka, ana Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara (MBA) ya Fedha na Uhasibu na Cheti cha IPSAS
Kazi yake kubwa ilijumuisha zaidi ya miaka kumi katika nyadhifa za usimamizi zinazohusisha michezo, fedha na usimamizi katika sekta za umma na binafsi, alitumia miaka mingi kufanya kazi kama Mkaguzi wa Ndani wa Serikali, mkurugenzi wa Utawala na fedha.