
DAR ES SALAAM: Mwanamitindo wa kimataifa, Miriam Odemba ametangaza kuanzisha jukwaa jipya la mitindo lijulikanalo kama Sauti ya Mitindo, litakalolenga kukuza vipaji vya wanamitindo wa kiume na wa kike nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Odemba amesema jukwaa hilo ni sehemu ya kurejesha mchango wake katika tasnia ya urembo baada ya kunufaika na fursa mbalimbali tangu alipoanza safari yake.
Amesema anatoka wilaya ya Temeke na mafanikio yake yametokana na juhudi pamoja na msaada wa watu mbalimbali waliomuamini tangu mwanzo.
Kwa sasa Odemba ni mama wa mtoto mmoja wa kike, Iris Piedimonte, ambaye amesema anaonesha kipaji cha urembo na michezo ya tenisi.
Aidha, alimshukuru Rita Paulsen kwa mchango wake mkubwa, akieleza kuwa tangazo alilowahi kutunukiwa na mwanamama huyo lilimfungulia milango ya mafanikio.
Odemba alikumbusha kuwa mwaka 1997 aliibuka mshindi wa Miss Temeke na baadaye kushinda Miss Tanzania, hatua iliyompa nafasi ya kuingia katika mashindano ya kimataifa.
Miongoni mwa mafanikio yake ni kushinda Face of Africa mwaka 1999 na kupata mkataba wa miaka mitatu na Elite Model Management, pamoja na kushika nafasi ya pili katika Miss East Africa mwaka 2000.
Pia alishinda taji la Miss Earth Air nchini Philippines na kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo nchini China.
Amesema kupitia Sauti ya Mitindo, kampuni yake itatafuta wanamitindo wa kiume, wa kike pamoja na plus size models, akitoa wito kwa wanaume kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo.
Katika hatua nyingine, Odemba amepongeza ujio wa mashindano ya Miss World yanayotarajiwa kufanyika nchini mwakani Mei, akisema ni fursa ya kuitangaza Tanzania kimataifa.




