Ligi Kuu

CCM Kirumba wapata uhuru

DAR ES SALAAM, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF limetangaza kuufungulia Uwanja wa CCM Kirumba uliopo jijini Mwanza kutumika kwa michezo ya ligi baada ya uongozi wa uwanja huo kufanya marekebisho yaliyokidhi vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.

Taarifa iliyotolewa na TFF imeeleza kuwa uwanja huo uliofungiwa kutokana na miundombinu yake kutofaa kutumika kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya Kanuni ya Leseni za Klabu umefunguliwa baada ya kukaguliwa na kuonekana kukidhi vigezo vya Kikanuni baada ya marekebisho yaliyoelekezwa kufanyika.

Kwenye taarifa hiyo pia TFF imeendelea kuzikumbusha klabu zinazoshiriki ligi kuu ya NBC kuendelea kuboresha na kutunza miundombinu ya viwanja vyao vya nyumbani kwa kushirikiana na wamiliki wa viwanja ikiwa klabu haimiliki uwanja wake yenyewe, ili michezo ya Ligi ichezwe kwenye viwanja bora vinavyosaidia kuongeza ushindani na thamani ya Ligi.

Ikumbukwe mapema Julai 15 mwaka jana rais wa shirikisho hilo Wallace Karia alisisitiza kuwa watakuwa wakali msimu huu hasa kwenye kanuni ya utunzaji wa viwanja ili kuendelea kupandisha ubora wa ligi kuu.

Related Articles

Back to top button