
KOCHA Mkuu wa Ruvu Shooting, Mbwana Makata, amesema kuwa hesabu zao ni kujiondoa mwisho wa msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Makata amesema wamejipanga kuondoka na pointi tatu watakaposhuka kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro Februari 24 kuikabili Kagera Sugar.
Ruvu Shooting wanaoshika mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 17, wako kwenye kipindi kigumu wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo uliopita kwa mabao 3-2 dhidi ya Geita Gold kwenye Uwanja wa Nyankumbu.
Akizungumza na HabariLEO, Kocha Makata amesema kuwa mchezo uliopita umewaonesha
mapungufu yao na tayari ameyafanyia kazi na hatakubali kupoteza tena kwani mipango yao ni kukusanya pointi katika michezo inayofuata wakianza na Kagera Sugar.
“Mechi hii ina umuhimu mkubwa kwetu tunatakiwa kushinda ili kurejesha hali ya kujiamini kikosini baada ya morali yetu kushuka tulipopoteza mchezo uliopita,” amesema Makata.

Naye Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, amesema kuwa baada ya kupata pointi tatu kwenye mchezo uliopita nguvu zao wanahamishia kwenye mechi dhidi ya Ruvu Shooting ingawa anaamini kuwa wataenda kukutana na upinzani mkubwa kutokana na mahitaji ya wapinzani wao.
“Naamini utakuwa mchezo mgumu, wapinzani wetu wanapambana kupata matokeo ya ushindi ili waweze kukaa sawa, lakini sisi tunahitaji kupata ushindi ili tuweze kusogea juu ya msimamo,” amesema Maxime.