Palmieri atua West Ham kwa Bil 41/-

KLABU ya West Ham United ‘The Hammers’ imemsajili beki wa kushoto Emerson Palmieri akitokea Chelsea kwa dili linaloaminika kuwa pauni milioni 15 sawa na shilingi bilioni 41,046,798,000.
Palmieri mwanasoka wa kimataifa wa Italia mwenye umri wa miaka 28 amejiunga na The Hammers kwa mkataba wa miaka minne.
Usajili huo una chaguo la kuongeza mkataba wa mwaka mmoja kwa pauni milioni 13 sawa na shilingi bilioni 35,573,891,600 pamoja na nyongeza ya pauni milioni mbili sawa na shilingi bilioni 5,472,906,400.
Palmieri aliitumikia Lyon kwa mkopo msimu uliopita na amepambana kupata namba kikosi cha kwanza Chelsea tangu alipohamia mwaka 2018 akitokea Roma.
“Siwezi kusubiri kuanza kucheza nikiwa na jezi ya West Ham. Nimefurahi sana kuwa hapa. Ni changamoto kubwa kwangu, ni timu kubwa, hivyo nina furaha sana kuwa hapa na niko tayari,” amesema Palmieri.
Palmieri ni mchezaji wa saba kusajiliwa West Ham United msimu huu.