Barker afichua nguvu ya Mo Dewji Simba

JOHANNESBURG: KOCHA Mkuu wa Simba, Steven Barker, amesema uwezo wa klabu hiyo kufanya maandalizi na safari za kimataifa ukiwa na kikosi kizima unatokana kwa kiasi kikubwa na msaada wa Rais wa klabu hiyo, Mohammed “Mo” Dewji, akisema amekuwa akitumia muda na rasilimali zake nyingi kwa ajili ya timu.
Akizungumza akiwa nchini Afrika Kusini Barker amesema si jambo rahisi kwa klabu kusafiri nje ya nchi ikiwa na wachezaji wote, benchi la ufundi pamoja na timu ya usaidizi, kutokana na gharama na rasilimali zinazohitajika kufanikisha safari hizo.
Amesema tangu alipowasili Simba, Mo Dewji amekuwa akitoa msaada mkubwa kwa timu, huku akiwa na mawasiliano ya mara kwa mara na kuonyesha shauku kubwa katika maendeleo ya klabu hiyo.
“Anatoa muda wake mwingi, rasilimali zake nyingi na nguvu zake kwa ajili ya timu, na naamini ni kwa sababu yake tunaweza kufanya mambo kama haya,” amesema Barker.
Kocha huyo amesema hata wanapokuwa nyumbani, Mo Dewji amekuwa akitoa ushirikiano mzuri katika maandalizi ya timu, huku akihakikisha mahitaji yanayowasilishwa kwa ajili ya kikosi yanapata msaada unaohitajika.
Barker amesema kwa kutambua mchango huo, jukumu la benchi la ufundi na wachezaji ni kuhakikisha Simba inajiandaa kwa kiwango bora na kutumia vizuri fursa inayotolewa na uongozi ili kufikia malengo ya klabu.




